banner

February 25, 2017

MAGEREZA KUJENGA KIWANDA CHA SUKARI

MAGEREZA KUJENGA KIWANDA CHA SUKARI

JESHI la Magereza limetiliana saini na Mifuko ya Hifadhi ya Jamii ya PPF na NSSF ili kufufua kilimo cha miwa na kiwanda cha sukari mkoani Morogoro kitakachozalisha zaidi ya tani za sukari 30,000 kwa mwaka.
Aidha, kiwanda hicho cha sukari kitaondoa tatizo la uhaba wa sukari nchini ambalo linatokea kila mwaka sambamba na kuondoa utegemezi wa sukari ambayo huagizwa kutoka nje ya nchi wakati ambao hakuna sukari ya kutosha nchini.
Akizungumza baada ya tukio hilo Dar es Salaam jana, Mkuu wa jeshi hilo, Juma Malewa alisema Machi Mosi mwaka huu kilimo cha miwa kitaanza katika eneo la gereza Mbigiri lililopo Morogoro.
Alisema kufufuliwa kwa kilimo cha miwa na pia kiwanda hicho cha sukari kinaendana na kauli ya Rais wa awamu ya tano, John Magufuli ya kuifanya Tanzania ya viwanda.
“Moja ya ahadi zake Rais ni kuifanya nchi yetu kuwa yenye uchumi wa viwanda, katika utekelezaji wa agizo hilo tulikutana na PPF na NSSF kwa mazungumzo ya kufufua kiwanda hiki,” alisema Malewa.
Mkurugenzi Mkuu wa mfuko wa Pensheni wa NSSF, Godias Kahyaara alisema kiwanda hicho kitazalisha tani 30,000 za sukari kila mwaka na kwamba tani zaidi ya 400,000 zitazalishwa katika kilimo cha miwa kwenye shamba hilo linalomilikiwa na Jeshi la Magereza.
“Mbali na kuzalisha sisi wenyewe, pia wakazi wa Dakawa watapata fursa ya kuuza miwa yao kiwandani, tunachowashauri wakae mkao wa kula kwa kuzalisha miwa ya kutosha kwaajili ya kuuza katika kiwanda hicho,” alisema Kahyarara.
Mkurugenzi Mkuu wa mfuko wa Pensheni wa PPF, William Erio alisema kiwanda hicho kitaokoa fedha za kigeni ambazo hutumika kila mwaka kwa ajili ya kuagiza sukari nje ya nchi.
Alitoa wito kwa wakazi wa maeneo jirani na kiwanda hicho kuongeza uzalishaji wa miwa kwaajili ya kuuza kiwandani ili kuchochea uchumi wao na pia kuongeza uzalishaji wa sukari kuhakikisha kwamba hakuna sukari inayoingizwa kutoka nje ya Tanzania.
Alisema ukarabati wa kiwanda hicho unaendelea na pia wanaendelea kusafisha mashamba ya miwa kwaajili ya kuanza kilimo Machi mosi mwaka huu.
Kwa mujibu wa Malewa, kiwanda hicho cha sukari kilianzishwa mwaka 1978 lakini kilifungwa mwaka 1996 kutokana na changamoto mbalimbali ikiwa ni pamoja na uchakavu wa mitambo na pia soko la sukari.

Whatsapp Button works on Mobile Device only

Start typing and press Enter to search