banner

February 08, 2017

VIROBA MWISHO SIKU 90 ZIJAZO

VIROBA MWISHO SIKU 90 ZIJAZO

SERIKALI inatarajia kupiga marufuku utengenezaji na uingizaji wa pombe za bei rahisi maarufu kama `Viroba' nchini ndani ya miezi mitatu ijayo sawa na siku 90.
Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dk. Hamisi Kigwangalla, aliyasema hayo bungeni mjini Dodoma juzi alipokuwa akijibu hoja za wabunge waliokuwa wakilalamikia kilevi hicho kutokana na kupunguza nguvu kazi ya Taifa wakati wa uwasilishwaji wa taarifa za Kamati ya Bunge ya Masuala ya Ukimwi na ya Huduma na Maendeleo ya Jamii kwa mwaka 2016/17.
Dk. Kigwangalla alisema kuwa baada ya miezi mitatu, kilevi hicho kitapigwa marufuku kutengenezwa au kuingizwa nchini pamoja na kuziba mianya yote ya uingizaji.
Alisema kilevi hicho hutumiwa na vijana wengi na hivyo kuharibu nguvu kazi ya Taifa.
Kwa upande wake, Mbunge wa Jimbo la Tarime Mjini Esther Matiko, amesema kwamba pombe hiyo inasababisha vifo vya vijana wengi nchini ambao ndio tegemeo kubwa na nguvu kazi ya Taifa.
“Katika kipindi hiki kifupi cha likizo yangu, nilikuwa jimboni kwangu na tumezika vijana wanne waliofariki dunia kutokana na matumizi ya viroba.
Hivyo wananchi wa jimbo langu wameniagiza kuja kulieleza Bunge athari za pombe hiyo ili tujadili na kuona namna gani ya kuliokoa Taifa hasa vijana kutoka katika janga hilo,” alifafanua Matiko.
Akiwasilisha taarifa ya Kamati, Mwenyekiti wa kamati hiyo, Dk. Faustine Ndugulile, alisema kuwa Kamati imebaini uwepo wa uhusiano mkubwa kati ya matumizi ya pombe hizo na kuongezeka kwa tabia hatarishi zinazochangia ongezeko la vijana katika matumizi ya dawa za kulevya.
Aidha, alisema hali hiyo inaathiri ufanisi wa nguvu kazi ya Taifa kutokana na madhara ya matumizi ya dawa za kulevya.
Hivyo Kamati imeishauri serikali kufungia kabisa uzalishaji na uuzwaji wa pombe hizo za viroba ili kulinusuru Taifa.

Post a Comment

Whatsapp Button works on Mobile Device only

Start typing and press Enter to search