banner

March 29, 2017

KALIDOU KOULIBALY AFICHA AIBU YA SIMBA WA TERANGA

KALIDOU KOULIBALY AFICHA AIBU YA SIMBA WA TERANGA

Beki wa klabu ya SSC Napoli ya Italia Kalidou Koulibaly, amelazimika kulipa gharamna za hoteli kwa ajili ya timu ya taifa ya Senegal ambayo ilikaribia kuzuia kwenye moja ya hoteli jijini London.
Beki huyo amelipa kiasi cha Pauni 20,000, baada ya shirikisho la soka nchini Senegal kuchelewa kufanya malipo kwenye hoteli hiyo, ambapo Simba wa Teranga waliweka kambi kwa ajili ya mchezo wa kimataifa wa kirafiki dhidi Nigeria.
Gazeti la L’Observateur limeripoti kuwa, shirikisho la soka nchini Senegal lilishindwa kulipa kwa wakati gharama za kuiweka timu ya taifa hotelini hapo kufuatia ukata unaowaandama kwa sasa.
Kwa kuzuia aibu ambayo huenda ingewakuta Senegal, Koulibaly akiwa na wakala wake Djily Djeng alizungumza na uongozi wa hoteli hiyo, na kukubali kubeba jukumu la kulipa gharama zote.
Koulibaly amechukua maamuzi hayo huku akiendelea kuhusushwa na mipango ya kusajiliwa na vinara wa ligi ya nchini England (Chelsea) kwa dau la Pauni milioni 60.
Katika mchezo wa kimataifa wa kirafiki uliohudhuriwa na mashabiki 2,013, Senegal walilazimishwa sare ya bao moja kwa moja dhidi ya Nigeria.
Mshambuliaji wa Manchester City Kelechi Iheanacho aliifungia Nigeria bao la kusawazisha, baada ya Moussa Sow kuifungia Senegal bao la kuongoza kipindi cha kwanza.

Post a Comment

Whatsapp Button works on Mobile Device only

Start typing and press Enter to search