banner

March 29, 2017

SIMBA WAKAMILIKA BUKOBA, KUIVAA KAGERA SUGAR J’PILI

SIMBA WAKAMILIKA BUKOBA, KUIVAA KAGERA SUGAR J’PILI

Nyota wa Burundi, Laudit Mavugo na wachezaji saba wa Simba waliokuwa na timu ya taifa ya soka ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars wamewasili Bukoba leo asubuhi kuungana na wenzao kwa ajili ya mchezo wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara Jumapili dhidi ya Kagera Sugar Uwanja wa Kaitaba, Bukoba.
Wachezaji wa Tanzania ni mabeki Mohammed Hussein ‘Tshabalala’, Abdi Banda, viungo Said Ndemla, Jonas Mkude, Shiza Kichuya, Muzamil Yassin na mshambuliaji Ibrahim Hajib ambao walibaki Dar es Salaam kuichezea Taifa Stars dhidi ya Botswana Jumamosi ikishinda 2-0 na dhidi ya Burundi jana ikishinda 2-1.
Nyota hao wanane tegemeo wa Wekundu wa Msimbazi wametua Bukoba kutekeleza wajibu wao kwa mwajiri wao, Simba SC ambaye atakuwa na kibarua kigumu Jumapili mbele ya timu ya kocha Mecky Mexime.
Wamewasili wakiongozana na Makamu wa Rais wa Simba SC, Geofrey Nyange ‘Kaburu’ ambaye pia ni Mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF).
Wamewasili kwa ndege ya shirika la Tanzania, ATCL wakiwa na mshambuliaji tegemeo wa Kagera Sugar, Mbaraka Yussuf ambaye naye alikuwa Taifa Stars.
Mbaraka Yussuf ndiye aliyefunga bao la ushindi jana Taifa Stars ikiichapa 2-1 Burundi, baada ya Simon Msuva kufunga la kwanza na Laudit Mavugo kuwasazishia wageni.

Post a Comment

Whatsapp Button works on Mobile Device only

Start typing and press Enter to search