banner

April 20, 2017

SIMBA YAAMUA KUFA NA MALINZI

SIMBA YAAMUA KUFA NA MALINZI

KUTOKANA na kuendelea kurindima kwa sakata la Simba kupewa pointi tatu dhidi ya Kagera Sugar ambao walimchezesha beki wao, Mohamed Fakhi anayedaiwa kuwa na kadi tatu za njano, klabu hiyo ya Msimbazi imeibuka na kulishutumu Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) wakidaiwa wanataka kuwahujumu wasitwae ubingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara msimu huu.
Akizungumza jana jijini Dar es Salaam kwenye mkutano wa waandishi wa habari, Msemaji wa Simba, Haji Manara, alisema klabu yao imegundua hujuma za waziwazi zinazofanywa na baadhi ya vigogo wa TFF.
Manara alimtaja Rais wa TFF, Jamal Malinzi, akidai anataka kuibeba Yanga kwenye mbio za ubingwa na sasa klabu hiyo ya Wekundu wa Msimbazi wamekaa mguu sawa kukabiliana nazo.
“Tuna taarifa za kile kikao cha kwanza cha Kamati ya Saa 72, mmoja wa viongozi wakuu wa TFF alitoa taarifa kwa mmoja wa maofisa wake akishinikiza matokeo yale yasitangazwe,” alisema Manara.
Msemaji huyo alisema walipopeleka suala la Fakhi kuchezeshwa akiwa na kadi tatu za njano hawakubahatisha, kwani walifuatilia wakafahamu kila kitu na pia Kamati ya Saa 72 ilipotoa maamuzi ya kuwapa pointi hizo tatu hawakukosea, hivyo suala hilo kupelekwa kwenye kamati nyingine ni mchezo mchafu unaotaka kufanywa.
“Siku zote Simba tuko makini na tunachokifanya, tulipopeleka malalamiko yetu kwamba Fakhi alichezeshwa akiwa na kadi tatu za njano, tulikuwa hatubahatishi, ndio maana Kamati ya Saa 72 ikaona mapungufu hayo ikatupa pointi tatu.
“Sasa tunashangaa kusikia kwamba kuna mkubwa mmoja alitaka kuizuia Kamati hiyo isitoe maamuzi yale, ila hawakutaka kuburuzwa na kufanya kazi yao kwa weledi. Yote hayo tunayajua na msione tupo kimya, tunaweza kufanya jambo kubwa,” alisema Manara.
Alisema kama watapokonywa pointi zao, hapatatosha kwa kuwa hawatakaa kimya, huku wakimtahadharisha Malinzi kuepuka kufanya upendeleo wowote ambao unaweza kuliingiza soka la Tanzania kwenye matatizo.
“Malinzi ni Mwenyekiti wa Chama cha Soka Mkoa Kagera, sasa haya mambo yanayoendelea yanatupa mashaka makubwa sana, niseme wazi nilikuwa namheshimu sana huyu mtu na hata mashabiki wa Simba walikuwa wakimheshimu sana, lakini haya anayoyafanya heshima ileile tuliyokuwa nayo kwake imeshuka kwa kiwango kikubwa.
“Hakukuwa na uhalali wa Kamati ya Sheria na Hadhi za Wachezaji ya Shirikisho la Soka la Tanzania kusikiliza suala hili, bali lilikuwa lirudishwe kwenye Bodi ya Ligi ili ifanye marejeo wala haikuhitaji ushahidi upya, utaratibu wa (majereo) ni kutumia ushahidi ule ule wa mara ya kwanza,” alisema Manara.
Manara alishangaa kamati hiyo ya sheria na hadhi kwa kumwita mchezaji huyo, akisema: “Inshangaza sana mchezaji anaitwa kuhojiwa, yaani mwizi anaulizwa eti umeiba, Mgosi (Mussa Hassan) alipokuwa anacheza Simba ilinyang’anywa pointi bila ya kuitwa popote, Erasto Nyoni naye hivyo hivyo.
“Kituko kingine unamwita mwamuzi wa akiba aliyetokea Mkoa wa Kagera kumhoji, huku akiwa hana ripoti, sasa atakwambia nini? Hii ni kutaka kuionea Simba.”
Pia msemaji huyo alizungumzia kitendo cha barua pepe za ripoti za waamuzi kudaiwa kufanyiwa uchunguzi wa makosa ya kimtandao (Cybercrime), ikidaiwa kwamba barua hizo za ‘zimefojiwa’.
“Hivi ripoti zote za waamuzi zimeshawahi kwenda Cybercrime? Kuna kesi pale? Ni kutuonea kulikovuka mipaka, kwanini isiende na  Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA)? Wanatakiwa kutuomba radhi kwa kutuhusisha na ‘kufoji’ barua pepe.
“Hivi unawezaje kuchezea barua pepe, wametukosea sana. Hivi unaweza kumchezea Boniface Wambura (Mwenyekiti wa Bodi ya Ligi), huku kutuonea kwa manufaa ya kuibeba Yanga tu,” aliongeza.
Manara alikumbushia kesi ya mshambuliaji wao wa zamani, Ramadhani Singano ambaye anachezea Azam.
“Yaani kesi yetu toka Julai mwaka 2015 hadi leo kimya, kamati hiyo hiyo iliyopeleka Cybercrime barua pepe ilituambia watapeleka kubaini ipi ni saini ya uongo ila mpaka leo hawajatujibu, lakini suala la Kagera limefanywa kwa umakini mkubwa.
Simba walikata rufaa TFF kwa madai ya Kagera Sugar kumchezesha Fahki akiwa na kadi tatu za njano katika mchezo uliomalizika kwa Wekundu hao wa Msimbazi kukubali kichapo cha mabao 2-1 Uwanja wa Kaitaba.
Shauri lao lilisikilizwa na Kamati ya Saa 72, ambapo waliigundua Kagera Sugar kutenda kosa hilo lakini baada ya maamuzi hayo, TFF waliamua kulirudisha Kamati ya Katiba, Sheria na Hadhi za Wachezaji ambapo mpaka sasa haijulikani mwisho wake.
BINGWA

Post a Comment

Whatsapp Button works on Mobile Device only

Start typing and press Enter to search