banner

April 22, 2017

UKODISHWAJI YANGA WAANZA UPYA

UKODISHWAJI YANGA WAANZA UPYA

ULE mchakato wa ukodishwaji wa klabu ya Yanga ambao awali ulikwama sasa umerudi upya ambapo Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dk. Harrison Mwakyembe, amepanga kukutana na viongozi wa klabu hiyo ili kuweka mambo sawa.
Mwenyekiti wa klabu hiyo kongwe nchini, alitoa pendekezo la kutaka akodishiwe timu hiyo kwa kipindi cha miaka 10, lakini mchakato wa kuelekea utekelezaji ulikwamana baada ya baadhi ya wanachama kupinga.
Awali Serikali kupitia Baraza la Michezo la Taifa (BMT), lilizuia michakato ya mabadiliko ya mifumo ya uendeshaji kwa klabu za Simba na Yanga kwa madai kwamba ulikuwa kinyume na katiba zao, lakini Dk. Mwakyembe ameanza kuufufua upya.
Katibu Mkuu wa BMT, Mohamed Kiganja, alitilia shaka na kupiga marufuku michakato hiyo baada ya baadhi ya wanachama wa klabu hizo kufungua kesi mahakamani kupinga michakato hiyo.
Taarifa za uhakika kutoka mjini hapa zinadai kuwa, Mwakyembe anataka kukutana na uongozi wa Yanga ili kuzungumzia suala hilo na kama mambo yataenda vizuri huenda mchakato huo ukaanza upya.
Mwakyembe ambaye alichukua nafasi ya Nape Nnauye, tayari amekutana na uongozi wa Simba na kuzungumza nao kuhusiana na jitihada zao za kutaka kubadili mfumo wa sasa kuwa wa hisa na sasa ni zamu ya Yanga.
Simba wanataka kumpa timu mfanyabiashara bilionea, Mohammed Dewji ‘Mo’ ambaye anataka kuwekeza hisa za asilimia 51 zenye thamani ya Sh bilioni 20.
Wanachama wa klabu hiyo wamepitisha kwa kauli moja mabadiliko ya katiba ya klabu hiyo na tayari yamewasilishwa kwa msajili wa vyama vya michezo kwa ajili ya kuidhinishwa.
Chanzo cha kuaminika kinadai kuwa baada ya juzi jioni Mwakyembe kukutana na viongozi wa Simba chini ya Rais wao Evance Aveva, sasa anawataka kukaa meza moja na Yanga.
“Kikao dhidi ya viongozi wa Simba, kilikuwa cha siri sana na mambo ya kule yamekuwa siri kubwa, nikudokeze tu mipango iliyopo waziri anataka kukutana na viongozi wa Yanga ili wazungumze kuhusu lile suala la ukodishwaji, akimaliza nadhani waandishi wataitwa na kuambiwa kilichojiri,” alisema kiongozi mmoja kutoka ofisi ya waziri huyo.

Post a Comment

Whatsapp Button works on Mobile Device only

Start typing and press Enter to search