Tangaza nasi

May 04, 2017

POINTI TATU ZA KAGERA HIZOO

NA ZAITUNI KIBWANA,
POINTI tatu za Ligi Kuu Bara ambazo Kagera Sugar ilipokwa na kupewa Simba kutokana na madai ya timu hiyo ya mkoani Kagera kumchezesha mchezaji mwenye kadi tatu za njano, kabla ya kurejeshwa kwa kikosi hicho kinachonolewa na Mecky Mexime, bado zinaonekana kuzagaa katika Mtaa wa Msimbazi yalipo maskani ya wakongwe hao wa soka nchini.
Pamoja na Kamati ya Sheria na Hadhi za Wachezaji ya TFF kuinyang’anya Simba pointi hizo ilizopewa na Kamati ya Saa 72 ya Shirikisho la Soka Tanzania, japo wakongwe hao wa soka nchini walifungwa mabao 2-1, jana klabu hiyo ilitangaza rasmi kutokubali kuona zikiyeyuka Msimbazi.
Katika hilo uongozi wa Simba umesema unasubiri barua kutoka Bodi ya Ligi ili wawasilishe malalamiko yao Shirikisho la Soka la Kimataifa (Fifa) kudai haki yao wakiamini Kamati ya Saa 72 haikuwa imekosea kuwapa pointi tatu za Kagera Sugar, kutokana na kumchezesha Mohammed Fakhi aliyekuwa ameshaonyeshwa kadi tatu za njano.
Rais wa Simba, Evans Aveva, amesema njia zipo nyingi za wao kupata haki yao, hivyo wanasubiri kupewa barua kutoka Bodi ya Ligi ambayo wataiambatanisha kwenda Fifa kudai haki yao.
“Tunajiuliza kwamba kanuni zinasemaje, mchezaji ni kweli ana kadi tatu za njano na Kamati ya Saa 72 ilifuata kanuni, sasa Kamati ya Sheria na Hadhi za Wachezaji imetupoka pointi zetu tulizopewa. Tunasubiri kupewa barua rasmi na Bodi ya Ligi kama ilivyotumwa awali ili tuweze kwenda mbele zaidi kudai haki yetu, tumefuatilia njia za kudai haki yetu tumeambiwa gharama inaweza kuanzia Dola 15,000, tupo tayari kulipa ili tupate haki yetu,” alisema Aveva.
Aveva alikwenda mbali zaidi kwa kusema kuwa watakwenda kwenye Mahakama ya Usuluhishi wa Michezo (CAS) ya Kimataifa (Fifa) ili kumaliza utata wa mchezaji wao aliyemaliza muda wake wa mkopo katika timu ya Kagera Sugar, Mbaraka Yusuph.
Akizungumzia maandalizi  yao ya mchezo wa  Kombe la FA dhidi ya Mbao, Aveva alisema wamejipanga vema kuhakikisha wanaibuka na ushindi kwenye mchezo huo ili kupata nafasi ya kushiriki michuano ya kimataifa.
“Awali tumepata kigugumizi mchezo wa fainali eti unafanyiwa droo na baadaye kubatilishwa na kupelekwa Dodoma, sisi tunarai moja tu kwa waendeshaji wa michuano hii, haya ni mashindano makubwa si jambo baya kama tukipewa taarifa za uwanja mapema itakuwa inaondoa minong’ono,” alisema.
Alisema wanawaheshimu wapinzani wao Mbao ila lazima wapokee kichapo kwenye mchezo huo.
“Mbao watatukuta pale Dodoma, tunawaheshimu sana Mbao lakini hatuwaogopi, nakumbuka goli la Mzamiru tulipocheza nao Mwanza, lilileta madhara baada ya watu kadhaa kupoteza maisha hivyo ni timu tunayoiheshimu sana, hata wangetupeleka CCM Kirumba au  Uwanja wa Nyamagana tungecheza na tupo tayari,” alisema.
Aveva alimaliza kwa kuzungumzia sakata la msemaji wao, Haji Manara ambaye kwa sasa amesimamishwa na Kamati ya Nidhamu ya Shirikisho hilo kutokana na madai mbalimbali ikiwamo kutoa lugha chafu kwa shirikisho hilo.
Aveva alisema tayari wamekata rufaa ili kuomba kusikilizwa kwa msemaji wao  ambaye awali kamati hiyo ilifanya maamuzi hayo bila hata ya kumsikiliza.
JIUNGE NA Bin RUWEHY SASA
Usipitwe!! Jiunge nasi kupitia Facebook, Twitter na Instagram ili kupata habari zote za Michezo! Usikose kujiunga na App Yetu Bonyeza HAPA kudownload applicationi ya Bin RUWEHY kwenye simu yako ili kupata habari zetu Haraka