banner

May 20, 2017

YANGA WAKABIDHIWA KOMBE LAO CCM KIRUMBA, MASHABIKI WAPAGAWA KWA FURAHA

YANGA WAKABIDHIWA KOMBE LAO CCM KIRUMBA, MASHABIKI WAPAGAWA KWA FURAHA

Hayawi hayawi hatimaye yamekuwa, Yanga imefanikiwa kukabidhiwa kombe la ubingwa wa Ligi Kuu ya Vodacom licha ya kufungwa bao 1-0 na Mbao FC kwenye Uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza.
Yanga imekabidhiwa ubingwa huo licha ya kulingana pointi na Simba ambao wameshika nafasi ya pili, lakini Yanga wana wastani mzuri wa mabao ya kufunga na kufungwa.
Yanga sasa itakuwa imefikisha kombe lake la 27 katika ligi hiyo huku wapinzani wao wa jadi, Simba wakiwa na mataji 18 ya ligi kuu, hivyo kuwafanya Simba kuwa na mlima mrefu kuwafikia wapinzani wao hao katika ulimwengu huo wa mataji ya ligi kuu.
Kutokana na kushika nafasi hiyo, Yanga imejihakikishia kucheza michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika inayoandaliwa na Shirikisho la Soka la Afrika (Caf) msimu ujao.
Mara baada ya mchezo dhidi ya Mabao, Yanga ikikabidhiwa kombe lake na kusababisha shangwe kuwa nyingi uwanjani hapo hasa kutoka kwa mashabiki ambao uvumilivu uliwashinda, wakaingia uwanjani walipokuwepo wachezaji wakikabidhiwa kombe hilo.
Ilibidi askari waliokuwepo uwanjani hapo kuingilia kuwasogeza pembeni mashabiki hao ambao walionekana wamepagawa na furaha.
Kwa mujibu wa kanuni za soka za Ligi Kuu ya Vodacom ni kuwa timu itakayotwaa kombe hilo mara tatu mfululizo, itapewa kombe hilo moja kwa moja. Hii ni mara ya tatu mfululizo kwa Yanga kutwaa kombe hilo.

Post a Comment

Whatsapp Button works on Mobile Device only

Start typing and press Enter to search