banner

May 19, 2017

YONDANI, KUIKOSA MBAO FC

MABINGWA watarajiwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara, Yanga, watamkosa beki wao, Kelvin Yondan, kwenye mchezo wao wa mwisho dhidi ya Mbao FC utakaopigwa kwenye Uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza.

Yanga inatarajia kuondoka leo kwa usafiri wa ndege na Nyondani atakosekana kutokana na kuwa na kadi tatu za njano, huku pia watamkosa mshambuliaji wao, Donald Ngoma ambaye bado anasumbuliwa na majeraha.
Akizungumza na BINGWA jana jijini Dar es Salaam, Meneja wa kikosi hicho, Hafidh Saleh, alisema licha ya kuwakosa wachezaji hao, lakini mshambuliaji wao, Simon Msuva atarejea.
Msuva aliukosa mchezo uliopita dhidi ya Toto Africans kutokana na jeraha alilolipata kwenye mchezo wao dhidi ya Kagera Sugar, lakini sasa amepona na ataweza kuungana na wenzake kwenye mchezo huo na Mbao.
“Kesho (leo) tunaenda Mwanza kwa ajili ya mchezo wetu wa mwisho dhidi ya Mbao, lakini tutawakosa Ngoma na Yondani ambao wana sababu tofauti, lakini tutakuwa nao kwenye msafara.
“Tutakuwa na Msuva ambaye tulimkosa kwenye mechi iliyopita ambayo alikuwa na majeraha na maandalizi mengine ya mchezo wenyewe ambao utakuwa wa kukabidhiwa kombe,” alisema meneja huyo.
Katika mchezo huo wa ugenini, Yanga inahitaji sare au ushindi wa namna yoyote ule ili kujikita zaidi kileleni na kujihakikishia kwa asilimia kubwa kutwaa ubingwa huo kwa mara ya tatu mfululizo msimu huu.

Post a Comment

Whatsapp Button works on Mobile Device only

Start typing and press Enter to search