banner

July 26, 2017

MICHUANO YA URIO CUP YAZINDULIWA KUNDUCHI, TIMU 32 KUSHIRIKI

MICHUANO YA URIO CUP YAZINDULIWA KUNDUCHI, TIMU 32 KUSHIRIKI

Michuano ya soka iliyopewa jina la Urio Cup itakayozishirikisha timu 32 kutoka maeneo mbalimbali ya Jiji la Dar es Salaam, imezinduliwa rasmi leo Jumatano na Diwani wa Kata ya Kunduchi, Michael Urio.
Michuano hiyo ambayo ina lengo la kuibua vipaji, inatarajiwa kuanza kutimua vumbi Agosti 7, mwaka huu kwenye Uwanja wa Shule ya Sekondari Tegeta jijini Dar.
Akizungumza wakati wa uzinduzi wa michuano hiyo, Diwani Urio amesema: “Michuano ya msimu huu inakuja tofauti, tumeongeza zawadi kwa washindi lakini pia tumepata wadau watakaotuunga mkono ambao ni Times FM, Msonge Afrika pamoja na Jomo International.
“Lengo la Urio Cup ni kuibua vipaji katika kata yetu ya Kunduchi na Dar es Salaam kwa jumla kwani michuano hii itazishirikisha timu zote kutoka maeneo mbalimbali lakini mechi zote zitachezwa huku Kunduchi kwa sababu tunataka kutoa hamasa kwa wakazi wa kata hii.”
Naye mratibu wa michuano hiyo, Deus Buliho, amesema: “Michuano itaanza Agosti 7 na itadumu kwa takribani miezi mitatu ambapo itaanzia hatua ya mtoano ambapo zitapigwa mechi za nyumbani na ugenini katika Uwanja wa Shule ya Sekondari Tegeta. Ada ya kiingilio kwa timu shiriki ni Sh 70,000.
“Kwa upande wa zawadi, bingwa atapata Sh milioni tatu na kikombe, mshindi wa pili Sh milioni moja na nusu, timu yenye nidhamu, mfungaji bora, kikundi bora cha ushangiliaji pamoja na kipa bora, hawa kila mmoja ataondoka na Sh laki moja, huku mchezaji bora wa mechi ‘man of the match’ akizawadiwa Sh 10,000.”
Buliho aliongeza kuwa, timu zote zitakazoingia hatua ya 16 Bora, zitazawadiwa jezi seti moja huku mashabiki wa soka watapata fursa ya kushuhudia mechi za michuano hiyo kwa kiingilio cha Sh 500.

Post a Comment

Whatsapp Button works on Mobile Device only

Start typing and press Enter to search