banner

August 31, 2018

SAMATTA MAMBO NI MOTO ATUPIA BAO,KRC GENK IKITINGA HATUA YA MAKUNDI EUROPA LEAGUE

SAMATTA MAMBO NI MOTO ATUPIA BAO,KRC GENK IKITINGA HATUA YA MAKUNDI EUROPA LEAGUE

Na Mwandishi Wetu, BRONDBY 
MSHAMBULIAJI wa kimataifa wa Tanzania, Mbwana Ally Samatta amekamilisha mchango mzuri kwa timu yake, KRC Genk kutinga hatua ya makundi y Europa League baada ya kufunga bao la nne katika ushindi wa 4-2 dhidi ya wenyeji, Brondby IF Uwanja wa Brondby nchini Denmark.
Genk inakwenda hatua ya makundi kwa ushindi wa jumla wa 9-4 baada ya kushinda 5-2 kwenye mchezo wa kwanza wiki iliyopita nchini Ubelgiji, Samatta akifunga mabao matatu peke yake.
Genk iliuanza vizuri mchezo wa leo ikipata mabao mawili ndani ya nusu saa, wafungaji kiungo wa Ukraine, Ruslan Malinovskiy dakika ya 14 na mshambuliaji Mkongo, Dieumerci N’Dongala dakika ya 32.
Lakini wenyeji wakazinduka na kusawazisha mabao yote hayo ndani ya saa moja ya mchezo, kupitia kwa mshambuliaji Mpoland, Kamil Wilczek dakika ya 34 na beki Msweden, Johan Larsson dakika ya 58.
Genk ikapata tena uhai na kufanikiwa kuongeza mabao mawili, la tatu akifunga beki Mbelgiji, Sebastien Dewaest dakika ya 66 na la nne Samatta dakika ya 87.  
Droo ya hatua ya makundi inatarajiwa kupangwa Leo  Agosti 31 ukumbi wa Grimaldi Forum mjini Monaco, Ufaransa na Genk ni miongoni mwa timu zinazoshika nafasi ya pili ya kwa ubora, maana yake itapangiwa wapinzani wawili hafifu, jambo ambalo litawaweka katika nafasi nzuri ya kwenda hata ya mtoano.
Kikosi cha Brondby IF kilikuwa: Schwabe, Jung, Kaiser, Mukhtar, Larsson, Wilczek/Laursen dk87, Vigen/Gammelby dk78, Radosevic/Tibbling dk45, Arajuuri, Kabongo na Erceg.
KRC Genk: Vukovic, Uronen, Lucumi, Dewaest, Maehle/Seigers dk78, Berge, Malinovskyi, Pozuelo/Piotrowski dk68, Trossard/Paintsil dk61, Ndongala na Samatta.

Whatsapp Button works on Mobile Device only

Start typing and press Enter to search