banner

October 15, 2019

NAMNA NDOA YA SAMATTA INAWEZA KUWA FUNDISHO KWA MASTAA

NAMNA NDOA YA SAMATTA INAWEZA KUWA FUNDISHO KWA MASTAA


Ndoa ya kepteni wa Timu ya Taifa ya Tanzania, Taifa Stars na KRC Genk ya Ubeligiji, Mbwana Samatta aliyofunga Alhamisi iliyopita na mpenzi wake wa siku nyingi; Neima Mgange, imeacha funzo kubwa kwa mastaa, Ijumaa Wikienda limedokezwa.

Baadhi ya mastaa waliozungumza na gazeti hili walionesha kushtushwa na tukio hilo na kwamba lilikuwa ni la ghafla mno.

Walisema kwanza, mbali na ndoa, lakini uhusiano wa Mbwana na Neima ulikuwa ni wa siri kubwa, tofauti na mastaa wengi hasa wa muziki na filamu Bongo ambao wakiwa na mpenzi tu huwa wanajionesha kwa kila mtu.

“Watu wengi wemekuwa na maswali kuwa aliweza vipi kumficha mpenzi wake huyo hali ya kuwa yeye ni staa wa kimataifa tofauti na mastaa wengine wa soka duniani ambao kimsingi huwa wanawaanika wachumba zao?

“Unajua sisi mastaa tumepata somo kubwa sana. Kama Mbwana angefanya ufahari kama wa baadhi ya mastaa Bongo, nakuhakikishia Dar isingepitika siku hiyo (Alhamisi iliyopita).

“Kwa jina na mkwanja wa Mbwana, angeweza hata kusimamisha mechi pale Uwanja wa Taifa (Dar), halafu akafunga ndoa yake kutokana na ustaa wake kwenye soka.

“Mimi nakwambia angekuwa msanii wa Bongo Movies, barabara zote za Dar zingefungwa kupisha msafara wake kuingia na kutoka Mlimani City. Nakuhakikishia ingekuwa balaa kubwa, lakini kwa Mbwana imekuwa simpo tu bila mbwembwe.

“Wewe fikiria ndiye Mtanzania pekee anayecheza Ligi ya Mabingwa Ulaya (UEFA), wewe unadhani angetaka kufanya mbwembwe ingekuwaje? Hawa akina Diamond wanapaswa kuiga alichokifa Mbwana na siyo kuwa kero kwa wengine.

“Naambiwa hata michango haikuwepo, kwa hiyo hakukuwa na mambo ya vikao vya harusi,” alisema mwigizaji Maurus Laurent ‘Ngubilu’.

Sherehe ya harusi ya Mbwana ilifanyika maeneo ya Kijichi-Mbagala jijini Dar na kuhudhuriwa na wachezaji wenzake wa Taifa Stars akiwemo Himid Mao na Thomas Ulimwengu.

Post a Comment

Whatsapp Button works on Mobile Device only

Start typing and press Enter to search