banner

October 15, 2019

YONDANI AWAGEUZIA KIBAO WAARABU

YONDANI AWAGEUZIA KIBAO WAARABU


Beki mkongwe na tegemeo wa Yanga, Kelvin Yondani, ametoa kauli ya kibabe kuelekea mchezo wao wa awali wa hatua ya mtoano wa Kombe la Shirikisho Afrika.

Yanga imepangwa kucheza na Pyramids FC ya nchini Misri katika michuano hiyo mikubwa Afrika mara baada ya Caf kuchezesha droo na timu hiyo kujikuta ikikutana na Waarab.

Timu hizo zinatarajiwa kujitupa kwenye Uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza Oktoba 27, mwaka huu katika mchezo unaotarajiwa kujaa upinzani mkubwa ambao Yanga wanahitaji ushindi mnono wa nyumbani.

Yondani alisema kuwa hakuna mchezaji yeyote mwenye hofu na wapinzani hao huku akiwataka mashabiki wa timu hiyo kuungana kwa pamoja katika kuisapoti timu kwa kuanzia mchezo wa nyumbani kabla ya kwenda ugenini.

Yondani alisema kuwa walitarajia kukutana na timu yoyote kabla ya droo hiyo kuchezeshwa, hivyo kwake amejiandaa kutimiza majukumu yake ya uwanjani ikiwemo kuokoa na kupunguza hatari golini kwao.

Aliongeza kuwa wamejiandaa kikamilifu kuhakikisha wanapata matokeo mazuri na hilo linawezekana kwao, licha ya kuondolewa kwenye Raundi ya Kwanza ya Ligi ya Mabingwa Afrika na Zesco United ya Zambia.

“Timu zote zilizofika hatua hii ni nzuri, tutajiandaa vizuri kuhakikisha tunapata matokeo mazuri, hatuwezi kurekebisha historia ya nyuma, lakini tunaweza kujiandaa kuweka historia mpya ya baadaye.

“Ninaamini historia hiyo itajengeka kwa kuwaondoa Waarab hao wanaopewa nafasi kubwa ya kutuondoa, hilo linawezekana kama kila mchezaji akitimiza majukumu yake.

“Safu ya ulinzi inatakiwa kulinda goli kwa kutoruhusu bao, viungo kuwachezesha washambuliaji ili wafunge mabao, kama kila mchezaji akitimiza hayo, basi hao Waarab tutawaondoa,” alisema Yondani.

Post a Comment

Whatsapp Button works on Mobile Device only

Start typing and press Enter to search