Tangaza nasi

July 26, 2017

DAKTARI WA YANGA AMFANYIA VIPIMO KABAMBA TSHISHIMBI

Kiungo wa Mbambane Swallows aliyekuwa akisakwa kwa nguvu kubwa na Klabu ya Yanga, Kabamba Tshishimbi amefanyiwa vipimo vya afya na inavyoonekana suala la kusaini mkataba mpya klabuni hapo lipo njiani.
Kabamba ambaye ni raia wa DRC Congo aliyekuwa akikipiga katika Klabu ya Mbambane Swallows ya Swaziland ameonekana akifanyiwa vipimo vya afya na Daktari Nassor Matuzya.
Katika picha hizo kiungo huyo anaonekana akipimwa pia urefu na baadaye kumshukuru Matyuza ambaye amekuwa akifanya kazi karibu na Klabu ya Yanga na amewahi kuwa daktari rasmi wa klabu hiyo mara kadhaa kipindi cha nyuma.

MAKUNDI YA LIGI DARAJA LA KWANZA (FDL)

Taarifa inayosambaa ni kuwa makundi kwa ajili ya Ligi Daraja la Kwanza yametoka na yanasomeka kama ifuatavyo: 
KUNDI A
1-Afrika Lyon (Dar) 
2-Ashati United (Dar) 
3-Friends Rangers (Dar) 
4-Jkt Ruvu (Pwani) 
5-Kiluvya United (Pwani) 
6-Mgambo JKT (Tanga) 
7-Mvuvunwa 
8-Polisi Moro (Moro) 

KUNDI B
1-Coastal Union (Tanga) 
2-Jkt Mlale (Ruvuma) 
3-KMC (Dar)
4-Mawezi Market (Moro) 
5-Mbeya Kwanza (Mbeya) 
6-Mshikamano (Dar) 
7-Mfundi United (Iringa) 
8-Polisi Dar (Dar) 

KUNDI C
1-Alliance School (Mwanza) 
2-Rinho Rangers (Tabora) 
3-Pamba (Mwanza) 
4-Polisi Mara (Mara) 
5-Polisi Dodoma (Dodoma) 
6-Transit Camp (Shinyanga) 
7-Toto African (Mwanza) 
8-JKT Oljoro (Arusha)

MICHUANO YA URIO CUP YAZINDULIWA KUNDUCHI, TIMU 32 KUSHIRIKI

Michuano ya soka iliyopewa jina la Urio Cup itakayozishirikisha timu 32 kutoka maeneo mbalimbali ya Jiji la Dar es Salaam, imezinduliwa rasmi leo Jumatano na Diwani wa Kata ya Kunduchi, Michael Urio.
Michuano hiyo ambayo ina lengo la kuibua vipaji, inatarajiwa kuanza kutimua vumbi Agosti 7, mwaka huu kwenye Uwanja wa Shule ya Sekondari Tegeta jijini Dar.
Akizungumza wakati wa uzinduzi wa michuano hiyo, Diwani Urio amesema: “Michuano ya msimu huu inakuja tofauti, tumeongeza zawadi kwa washindi lakini pia tumepata wadau watakaotuunga mkono ambao ni Times FM, Msonge Afrika pamoja na Jomo International.
“Lengo la Urio Cup ni kuibua vipaji katika kata yetu ya Kunduchi na Dar es Salaam kwa jumla kwani michuano hii itazishirikisha timu zote kutoka maeneo mbalimbali lakini mechi zote zitachezwa huku Kunduchi kwa sababu tunataka kutoa hamasa kwa wakazi wa kata hii.”
Naye mratibu wa michuano hiyo, Deus Buliho, amesema: “Michuano itaanza Agosti 7 na itadumu kwa takribani miezi mitatu ambapo itaanzia hatua ya mtoano ambapo zitapigwa mechi za nyumbani na ugenini katika Uwanja wa Shule ya Sekondari Tegeta. Ada ya kiingilio kwa timu shiriki ni Sh 70,000.
“Kwa upande wa zawadi, bingwa atapata Sh milioni tatu na kikombe, mshindi wa pili Sh milioni moja na nusu, timu yenye nidhamu, mfungaji bora, kikundi bora cha ushangiliaji pamoja na kipa bora, hawa kila mmoja ataondoka na Sh laki moja, huku mchezaji bora wa mechi ‘man of the match’ akizawadiwa Sh 10,000.”
Buliho aliongeza kuwa, timu zote zitakazoingia hatua ya 16 Bora, zitazawadiwa jezi seti moja huku mashabiki wa soka watapata fursa ya kushuhudia mechi za michuano hiyo kwa kiingilio cha Sh 500.


SINGIDA UNITED WAAMUA KUHAMISHIA MAJESHI MJINI DODOMA KWA MUDA

Uongozi wa Klabu ya Singida United, umesema kuwa, wamepanga mechi zao za kwanza za nyumbani za Ligi Kuu Bara wachezee kwenye Uwanja wa Jamhuri, Dodoma kutokana na uwanja wao wa Namfua kutokuwa tayari.

Mechi ambazo timu hiyo inaweza kucheza mkoani Dodoma ni dhidi ya Mbao iliyopangwa kupigwa Septemba Mosi pamoja na ile dhidi ya Stand United ambayo katika ratiba inaonyesha itachezwa Septemba 9. Mechi hizo zote zilitakiwa kupigwa katika Uwanja wa Namfua ambao bado upo kwenye matengenezo makubwa.

Katibu wa klabu hiyo, Abdulrahman Sima, amesema: “Uwanja wetu wa Namfua bado haujakamilika na sidhani kama ligi ikianza utakuwa tayari kutumika, marekebisho yanayofanywa ni makubwa, zile nyasi zilizopandwa zinaendelea kuota japo itakuwa haraka sana kuutumia.

“Kutokana na hali hiyo, tumeliomba Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) ,kuturuhusu kuutumia Uwanja wa Jamhuri uliopo Dodoma kwa mechi zetu za awali za nyumbani mpaka pale uwanja wetu utakapokuwa tayari na TFF wamekubali ombi letu.”


Timu hiyo ambayo imepanda daraja hivi karibuni, Agosti 26, mwaka huu itaanza mechi yake ya Ligi Kuu Bara ikiwa ugenini kucheza dhidi ya Mwadui FC kwenye Uwanja wa Mwadui Complex.

MSUVA KUONDOKA DAR JUMATANO HII KUELEKEA MOROCCO

Winga wa Yanga, Simon Msuva anatarajiwa kuondoka jijini Dar es Salaam, Jumatano ya Julai 26 kwa ajili ya kwenda nchini Morocco kukamilisha mchakato wa uhamisho wake kujiunga na timu ya Difaa Hassani El-Jadida inayoshiriki Ligi Kuu ya Morocco.
Difaa ambayo imeshamsajili Mtanzania mwingine, Ramadhani Singano kutoka Azam FC, iko tayari kutoa dola 150,000 kumsajili Msuva ambaye amebakiza miezi tisa katika mkataba wake Yanga.
Imeelezwa kuwa Msuva ameshafuzu vipimo vya afya na akifika Morocco anatarajiwa kusaini moja kwa moja mkataba wa kujiunga na timu hiyo.
Msuva alishindwa kwenda Morocco tangu wiki jana kwa kuwa alikuwa Kigali, Rwanda kwa ajili ya majukumu ya timu ya taifa ya Tanzania uliyokuwa ikiwania tiketi ya kucheza michuano ya Afrika kwa Wachezaji Wanaocheza Ligi za Ndani (CHAN). 

REAL MADRID KUWEKA KUFURU KWA MBAPPE, WAKUBALI KUMSAJILI KWA PAUNI 160M

Inadaiwa Real Madrid imekubali kumsajili Kylian Mbappe kutoka Monaco kwa pauni 160m, italipa pauni 143, kisha 17m itakuwa nyongeza katika mkataba.
Ikiwa taarifa hizo zitakuwa na ukweli na dili hilo litakamilika, inamaana kuwa kuna Real Madrid itakuwa inaandika rekodi ya kuwa klabu iliyotoa fedha nyingi kusajili mchezaji mmoja.
Rekodi ya sasa ya mchezaji aliyesajiliwa kwa dau kubwa duniani inashikiliwa na Paul Pogba ambaye alisajiliwa kwa pauni milioni 89 kutoka Juventus kwenda Manchester United.
Mbappe amekuwa akiwindwa na klabu nyingi kubwa za Ulaya, hivyo kama ni kweli Madrid wanataka kuweka dau hilo, inamaanisha kuwa wamezifukuza klabu zote katika dili hilo ili wabaki wao tu. 

MATOLA KAAMUA, ATEMA WACHEZAJI 10, ASAJILI 10 LIPULI FC

Kocha mpya wa Lipuli FC, Selemani Matola amezungumza juu ya mikakati yake ya kuijenga upya timu hiyo ambapo amesema ana mipango ya kuongeza wachezaji 10 wapya.
Matola ambaye ni kiungo na kocha wa zamani wa Simba, amesema kuwa usajili huo wa wachezaji 10 unatokana ripoti ya kocha aliyepita ambayo aliikabidhi klabuni hapo.
Amesema kutakuwa na wachezaji 10 wapya, pia walioipandisha timu nao watabaki 10 na wachezaji watano watapatikana kutokana na majaribio ambayo wamekuwa wakiyafanya kikosini hapo.
Hivyo, jumla Lipuli FC itakuwa na wachezaji 25 katika msimu ujao wa 2017/18, lakini amedai kuwa usajili huo utategemea na mwongozo wa uongozi wake wa Lipuli FC.

BOCCO AJIUNGA RASMI NA KAMBI YA SIMBA SAUZI

Mshambuliaji wa timu ya Taifa ya Tanzania na Wekundu wa Msimbazi Simba, amejiunga rasmi na kambi ya timu hiyo iliyo Afrika Kusini kwa ajili ya maandalizi ya msimu wa 2017/18 wa ligi kuu ya Vodacom.

YANGA SAFARINI MOROGORO, KUWEKA KAMBI YA SIKU 7

Kikosi cha Yanga  kinatarajiwa kuondoka jijini Dar es Salaam mchana wa leo Jumatano kuelekea Morogoro kwa ajili ya kuendeleza mchakato wa kujiandaa kwa msimu ujao wa 2017/18.
Yanga ambao ni mabingwa hao wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara wanatarajiwa kuwa kambini mkoani Morogoro kwa muda wa siku saba kujiandaa na michezo miwili ya kirafiki itakayopigwa Agosti 6 na 12, mwaka huu.
Ofisa Habari wa Yanga, Dismass Ten amethibitisha juu ya safari hiyo kwa kusema kocha wao mkuu, George Lwandamina anatarajiwa kuitumia kambi hiyo kukiandaa kikosi chake vizuri ambapo msimu huo unaokuja kinatarajiwa kushiriki katika Ligi ya Mabingwa Afrika.

YANGA YATANGAZA KUMSAJILI KIPA WA SERENGETI BOYS, ASAINI MIAKA MITANO

Ramadhani Kabwili.
Baada ya tetesi ndani ya wiki kadhaa, hatimaye Klabu ya Yanga imetangaza kumsajili kipa chipukizi, Ramadhani Kabwili.
Kipa huyo aliyekuwa akiidakia timu ya taifa ya vijana chini ya umri wa miaka 17, Serengeti Boys amesaini mkataba wa miaka mitano kuitumikia klabu hiyo yenye makao makuu mitaa ya Jangwani jijini Dar es Salaam.
Kabwili anaungana na kipa mwingine mpya, Mcameroon Youthe Rostand aliyesajiliwa kutoka African Lyon na Benno Kakolanya ambaye huu utakuwa msimu wa pili tangu asajiliwe akitokea Tanzania Prisons ya Mbeya.
Kabwili na Rostand wote wanasajiliwa kuchukua nafasi za makipa wa muda mrefu wa Yanga, Ally Mustafa ‘Barthez’ na Deogratius Munishi ‘Dida’ waliomaliza mikataba yao na kuruhusiwa kuondoka.