banner

February 27, 2017

PLUIJM: NIMEUMIZWA NA KICHUYA

PLUIJM: NIMEUMIZWA NA KICHUYA

MKURUGENZI wa Ufundi wa Yanga, Hans van der Pluijm, ameumizwa na kipigo cha mabao 2-1 walichokipata kutoka kwa mahasimu wao, Simba katika mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara uliochezwa juzi kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Pluijm aliyeiongoza Yanga kwa mafanikio makubwa mwanzoni mwa msimu, uongozi wa  klabu hiyo ulifanya mabadiliko katika benchi la ufundi kwa kumwajiri George Lwandamina kuwa kocha mkuu na Pluijm kupandishwa cheo.
Hata hivyo, Pluijm amesema ameumizwa sana na matokeo hayo hasa bao la pili ambalo ndilo limewanyang’anya japo pointi moja kwenye mchezo huo na kwamba bao hilo la Shiza Kichuya limeharibu mipango yao ya kutwaa ubingwa msimu huu.
Pluijm alisema kwa upande wake kama Mkurugenzi wa Ufundi wa timu hiyo, ameyapokea kwa masikitiko makubwa matokeo hayo kwani yana athari kubwa sana katika mbio zao za kutetea ubingwa.
“Ni matokeo mabaya, kufungwa si jambo zuri kwa timu yetu kwa sasa. Tumejipanga kutetea ubingwa wetu msimu huu, lakini kwa bahati mbaya tumepoteza mchezo wetu na Simba. Inauma lakini hakuna jinsi, tunajipanga kwa michezo ijayo,” alisema Pluijm.
Akiuzungumzia mchezo huo, Mholanzi huyo alisema kwa nafasi yake hawezi kusema chochote kuhusiana na masuala ya kiufundi na amewaachia wenye dhamana hiyo kuzungumzia kilichotokea.
“Siwezi kuzungumza chochote kuhusu mambo ya kiufundi kwani nikifanya hivyo nitakuwa nimeingilia majukumu ya benchi la ufundi, kitu ambacho si sahihi,” alisema Pluijm.
Pluijm alisisitiza kuwa hakuna hata Mwanayanga mmoja ambaye atakuwa amefurahishwa na matokeo hayo, hasa ukizingatia moja ya mikakati yao msimu huu ni kuifunga Simba na kutetea ubingwa wao wa Ligi Kuu Tanzania Bara.

Whatsapp Button works on Mobile Device only

Start typing and press Enter to search