banner

September 21, 2019

TIWAAMBIE KIBA, MONDI WARUDI NYUMBANI KUMENOGA AU?

TIWAAMBIE KIBA, MONDI WARUDI NYUMBANI KUMENOGA AU?


SIKU za hivi karibuni upepo wa mastaa wa kiume hususan wa Bongo Fleva kuwa na mahusiano au kuoa wanawake kutoka nje ya Bongo umekuwa ukivuma kwa kasi.

Imetokea kwa Ambwene Yesaya ‘AY’ ambaye ameoa mtoto mzuri Remy kutoka pale Rwanda, kabla ya kuoa mwanamke huyo, AY alikuwa na uhusiano na mwanadada Cecialia Wairimu ‘Amani’ kutoka Kenya lakini baadaye walimwagana.

Upepo huo haukumuacha salama pia mkali wa Bongo Fleva, Ali Saleh Kiba ‘AliKiba’ ambaye naye alizunguka weee, mwishoni akaangukia mikononi mwa Amina Khalef kutoka Kenya, wakafunga ndoa Aprili, mwaka jana.

Huku na huku Ben Pol naye akapiga jaramba weee kwa wanawake wa Kibongo, mwisho wa siku akatulia kwa mtoto wa Kikenya, Anerlisa. Maisha yanaendelea mpaka sasa na tayari wameshavalishana pete, wanaelekea kwenye ndoa.

Vivyo hivyo kwa Nasibu Abdul ‘Diamond Platnumz’ ambaye kabla ya kutulia kwa mrembo wa Kikenya, Tanasha Donna, alifanya ‘mazoezi’ kwa warembo kadhaa wa Kibongo kisha kuangukia kwa Mganda Zarinah Hassan ‘Zari The Boss Lady’ ambaye alizaa naye watoto wawili kisha wakaachana.

Harmonize naye kawaangalia kaka zake akaona kama kuna kitu wanafaidi hivi, naye akajivutia kifaa chake kutoka nchini Italy, ametulia nacho mpaka sasa na tayari wameshafanya taratibu za awali na wanakoelekea ni kukamilisha michakato ya ndoa.

Ukiachana na vijana wetu hawa kuonekana kujituliza kimahaba kwa warembo kutoka nje ya nchi, maswali mitandaoni yamekuwa ni kwa nini hasa vijana wetu wamekuwa wakikimbilia zaidi nje ya nchi na si warembo wazawa?

Watu wanajiongeza sana na wengine kuhisi labda pengine warembo kutoka nje ya nchi wana uvumilivu na kujua kujituliza na wanaume tofauti na wanawake wa Kibongo. Sitaki kuamini katika hilo lakini naheshimu mawazo yao.

Lakini pamoja na hayo, tumeshuhudia pia baadhi ya vijana wetu wakikwama kuendelea na mahusiano na haohao warembo wa kutoka nje ya Bongo. Kwa upande wa Diamond tumeona yaliyotokea kwa Zari, sarakasi zilikuwa nyingi lakini mwisho wa siku waliamua kuachana.

Kuachana kwa Mondi na Zari kulikuwa na uzito sana hasa kwa kuzingatia wawili hawa tayari walishakuwa na ‘bondi’ ya watoto. Lakini mwisho wa siku wakaamua kuachana, kila mmoja akaanzisha mahusiano mapya.

Diamond kwa mara nyingine akaingia kwenye mahusiano na mrembo kutoka Bongo, kawaacha tena wazawa! Yaliyomtokea Diamond kwa Zari, yanatajwa pia kumtokea Kiba kwa Amina ambaye walifunga ndoa ya kidini kabisa.

Licha ya wenyewe kutozungumza lakini madai ya ndoa yao kuvunjika yana uzito wa hali ya juu na dalili zinaonesha kwamba kuna viashiria vya ndoa hiyo kuwa kwenye hali mbaya hata kama itakuwa bado ingali hai.

Madai yamekuwa mengi ya kwamba ndoa hiyo imeota mbawa, watu wanashusha shahidi mbalimbali za kimazingira zinazoashiria kwamba ndoa hiyo imevunjika. Mfano wameonesha video ambayo mtoto wa Abdu Kiba amefanyiwa sherehe ya kuzaliwa nyumbani kwa Kiba lakini Amina haonekani kwenye hiyo video, wanaonekana wanawake wenginewengine tu.

Lakini kama hiyo haitoshi wapo majirani wa Kiba ambao wanadai kuwa hawajamuona shemeji yao nyumbani hapo kwa muda mrefu sasa. Kuna madai mengine mitandaoni yanaeleza kuwa Kiba ameshampa talaka tatu mkewe huyo.

Ni dhahiri kabisa madai hayo Kiba ameyaona na kwa namna moja au nyingine, ameshindwa kuyajibu. Yawezekana yakawa na ukweli ndiyo maana kanyamaza au pengine hayana ukweli na yeye ameamua kuyapuuzia.

Baada ya kuona madai hayo yakiwa na uzito wa hali ya juu na Kiba amekaa kimya hataki kuyazungumzia, baadhi ya mashabiki mitandaoni wamejiongeza kwa kuyaamini na kudai eti pengine Kiba angeangalia upande wa pili yaani nyumbani kwani kuna warembo wazuri tu wa kuoa.

Kwamba hata Mondi kama alishindwa kwa Zari, na ikitokea ameshindwa kwa Tanasha basi wana kila sababu ya kurejea nyumbani kwani kuna wanawake wazuri wa sura na tabia wanaojua misingi ya ndoa na thamani ya mwanaume.

Licha ya watu hao kutoa maoni yao, kwangu mimi bado naamini maisha ni popote. Kuoa au kuolewa mtu anaweza kutimiza jambo hilo mahali popote iwe ndani au nje ya nchi. Suala la msingi la kuangalia ni kuendana kitabia na kuishi kwa amani na upendo!

Post a Comment

Whatsapp Button works on Mobile Device only

Start typing and press Enter to search