banner

January 19, 2020

MAMBO 7 YANAYOILAZIMISHA ASTON VILLA INAMPATA NA KUMTUMIA SAMATTA

MAMBO 7 YANAYOILAZIMISHA ASTON VILLA INAMPATA NA KUMTUMIA SAMATTA






Na Saleh Ally
KOCHA Dean Smith wa Aston Villa ndiye aliyemchagua mshambuliaji Mbwana Samatta kutoka KRC Genk kujiunga na kikosi chake kwa ajili ya ukombozi kuhakikisha wanabaki Ligi Kuu England.

Samatta anakwenda kuandika rekodi nyingine mpya ya kuwa Mtanzania wa kwanza kucheza Premier League, yaani ligi kubwa na maarufu kuliko nyingine duniani.

Wakati Samatta anakwenda Aston Villa, kutakuwa na hesabu ya mambo mengi sana kama rekodi mpya na kadhalika lakini kikubwa cha kujiuliza ni kuwa ataweza kupata nafasi ya kucheza katika ligi hiyo? Bila shaka, jibu ni ndiyo.

Nasema ni ndiyo kwa mambo takriban saba ambayo yanaonyesha ni lazima Samatta apate nafasi katika kikosi cha kwanza.

MOJA:
Lazima Samatta apate namba kwa kuwa Kocha Dean ndiye aliyemchagua Samatta akiamini ana nafasi ya kumpatia kile kinachomsumbua kwa muda tangu ametua hapo.
Dean anataka mabao ya kufunga kwa ajili ya kukusanya pointi na unaona katika mechi nane za mwisho, wamepoteza sita jambo linalowafanya wazidi kubaki mkiani mwa EPL. Kwa sasa wako nafasi ya 18 katika timu 20.


PILI:
Kuumia kwa mshambuliaji tegemeo wa Aston Villa, Wesley ambaye analazimika kuwa nje kwa msimu mzima, bila shaka ni nafasi kwa Samatta na lazima kocha atataka kumtumia.

Kwa timu kama Aston Villa ambayo inapambana kuepuka kuteremka daraja, kama ingeona hakuna nafasi ya kujikomboa, isingekubali kutoa fedha hizo kwa kuwa ni nyingi kwao.
Kuzitoa, maana yake wanajua zitakuwa na msaada kwa maana ya anayekuja lazima awe sehemu ya msaada wa ukombozi kubaki EPL.

Wastani wa 1.95 kufunga bao katika mechi bado si mzuri, unapaswa kuongezeka angalau hadi 2.55 ili Aston Villa isimame salama na uhakika wa kubaki katika ligi hiyo kubwa duniani.

Mfano, angalia wastani wa kufungwa mabao katika mechi ni 2.63. Hii inaonyesha bado wana nafasi ya kufungwa zaidi kuliko kufunga na Dean ndio anachofanya kuhakikisha kinabadilika ili kuepuka msitari mwekundu wa kuteremka daraja.

TATU:
Aston Villa wamebakiza mechi 17 na ya kwanza dhidi ya Brighton leo, Samatta ataikosa na sababu kuu ni kwa kuwa bado atakuwa hajapata kibali cha kufanya kazi nchini England.

Maana yake zitabaki mechi 16 za EPL ambazo Samatta kama atakuwa fiti atakuwa na nafasi ya kucheza.

Katika mechi hizi 16 zilizobaki, nyingi zitakuwa za nyumbani ambako watakuwa na sapoti kubwa.

Lazima Dean atamtumia Samatta katika mechi 10 za nyumbani kwa kuwa bado hajawa na presha kubwa kwa kawaida kisaikolojia, wachezaji wapya huwa hawana presha kubwa ya mashabiki kama wale waliozoea.

Katika mechi nyingi za Genk, Samatta alionekana kufanya vizuri zaidi nyumbani. Bila shaka, kwa Dean hatakuwa na kipingamizi katika hilo.


 NNE:
Katika mahojiano yake hivi karibuni, Dean alisema wanahitaji mshambuliaji mwenye kasi kwa kuwa kikosi chake kinapocheza kwa kasi kinakuwa hatari zaidi.

Mechi ya mwisho walitunguliwa kwa mabao 6-1 wakiwa nyumbani dhidi ya Manchester City. Lakini walikuwa wametoka kuitwanga Burnley kwa mabao 2-1, kabla walipoteza kwa mabao 3-0 wakiwa ugenini dhidi ya Watford.

 Samatta ana kasi, huenda Premier League kitakuwa kipimo chake sahihi kwa kuwa ni mchezaji mwenye kasi, mwepesi kuliona lango kwa maana ya uamuzi wa haraka, kitu ambacho kimekosekana katika safu ya ushambulizi ya Aston Villa.

TANO:
Kweli mabao yataiinua Aston Villa kutoka ilipo na lazima yawe mengi ili kutengeneza pointi na hasa tatu, yaani ushindi.

Mabao mengi ni muhimu pia katika suala la Goal Difference (GD) maana kuna wakati inakuwa na umuhimu. Ushindi mkubwa wa mwisho wa Aston Villa ulikuwa ugenini dhidi ya Norwich, ilikuwa ni Oktoba 5, 2019 waliposhinda kwa mabao 5-1.

 Tokea hapo, hawajawahi kufunga hata mabao matatu katika mechi moja tu. Hii unaona ni maana nyingine ya Dean kuhakikisha anampata Samatta na anacheza.

Hakuna ubishi, Samatta ni mchanga katika EPL lakini anatua na kuvishwa jukumu kubwa sana ambalo kama ataliweza, bila shaka thamani yake itapanda maradufu kwa kuwa timu zote zinajua mzigo mzito zaidi ya ule wa Mnyamwezi walionao Aston Villa katika kipindi hiki.

SITA:
Katika mechi za nyumbani, mara chache hawajafunga hata kama watashindwa. Inaonekana ni 9% ndio wanaweza wasifunge nyumbani. Lakini ugenini, inaonekana hawana uhakika na mechi nyingi wametoka bila ya kuwa na bao.



SABA:
Dean ana presha kubwa sana ya kutaka ushindi kwa kuwa anajua anatakiwa angalau pointi 10 tu katika mechi nne ili ajikomboe mapema na kuteremka daraja.

Angalia Aston Villa wako katika nafasi ya 18 wakiwa na pointi 21 lakini timu zilizo katika nafasi ya 17-Watford, 16-West Ham, kila moja ina pointi 22 na nafasi ya 15-Burnley na 14-Brighton, kila moja ina pointi 24. Maana yake ushindi mara mbili mfululizo, lazima utaing’oa Aston Villa mkiani.



Hivyo ili kung’oka ni lazima kuwa na ushindi na ushindi unasababishwa na mabao na ulinzi bora. Aliye na mabao hayo au anayeweza kusababisha ni Samatta na Dean bila ya ubishi amemuamini, bila shaka lazima atacheza.



Dean si kocha mkubwa sana, Aston Villa ndio timu yake kubwa ya kwanza. Maana yake ana uwezo mkubwa wa kuwajua wachezaji aina ya Samatta kwa kuwa amekuwa akifundisha timu zenye madaraja ya chini kabla ya kutua Aston Villa.





Hivyo kwake, haiwezi kuwa suala gumu kuamini uwezo wa Samatta pamoja na ugeni wake katika Premier League.

Hamu ya Watanzania wengi ni kumuona mchezaji wa kwanza Mtanzania akiwa na uzi wa timu ya Premier League akiitumikia.

Samatta ana kiu ya kuvaa jezi ya timu ya Premier League na kutimiza ndoto yake lakini kuonyesha alichonacho anachoamini kitafanya kazi Premier League.

Kwa nilivyozungumza na waandishi wa Aston Villa, wamenithibitishia ni uhakika Samatta anatua katika kikosi chao na ishu kubwa ni kibali cha kazi huenda kitamzuia kucheza mechi ya leo lakini ana nafasi kubwa ya kuanza kazi rasmi mechi itakayofuatia na hii ndoto na kiu ya Watanzania, itakuwa imepata wa kuikata.







Post a Comment

Whatsapp Button works on Mobile Device only

Start typing and press Enter to search