Tangaza nasi

February 14, 2020

SI SAWA, NI HATARI SANA WACHEZAJI KUCHANGANYIKA NA MASHABIKI KAMA ILIVYOKUWA JAMHURI
Na Saleh Ally
MATATIZO mengi huanza kutokea kwanza na baada ya hapo watu huanza kutafuta utatuzi wake, wakati ilikuwa inawezekana kupatikana kwa utatuzi hata kabla ya tatizo kutokea.


Kwa nini tatizo linatokea na lingeweza kupatiwa utatuzi kabla? Hii ni kutokana na mambo kupelekwa kwa mazoea au watu kung’amua kuna tatizo lakini baadaye wakahisi hakutakuwa na tatizo.


Neno kuhisi ndilo linakuwa chanzo cha tatizo kuu kwa kuwa wahusika waliona, halafu wakahisi hakutakuwa na tatizo. Kutokana na kuhisia basi wakaamua kunyamaza bila ya kufanya jambo lolote. Hii ni hatari sana.


Baada ya mechi kati ya Simba na Mtibwa Sugar kwenye Uwanja wa Jamhuri, Morogoro, juzi, mashabiki walivamia uwanjani kwa kiwango kikubwa.


Wengi wao wakiwazunguka wachezaji, wengi wakionekana kuimba nyimbo za kuwasifia kama ilivyokuwa kwa Hassan Dilunga.


Mashabiki hao walifaya hata mahojiano kati ya wachezaji na makocha na vyombo vya habari kuwa magumu sana. Kwani hata wakati wakihojiwa, wako walirukaruka kwa nyuma, wengine wakiwasukuma hata wanaohojiwa hadi Polisi walipolazimika kuanza kuwafukuza na kuweka uzio wa maelekezo.


Wakati nikijadili na mtu mmoja, mfano wake ulikuwa ni wale mashabiki wa Aston Villa walioingia uwanjani baada ya mechi ya nusu fainali ya pili ya Carabao Cup. Villa walishinda mechi hiyo kwa mabao 2-1 na kutinga fainali ambapo itacheza dhidi ya Manchester City.


Mara tu baada ya mechi, mashabiki waliingia uwanjani na kuanza kusherehekea na wachezaji wakiwabeba na kadhalika. Rafiki yangu tuliyekuwa tukibadilishana mawazo, aliona hilo jambo kama linatokea Ulaya, kwetu haliwezi kuwa vibaya.


Hakika hata Ulaya limetokea, halikuwa ni jambo zuri na wao waliliona kwa kuwa mpira una utaratibu wake na mashabiki wanatakiwa kusherehekea wakiwa jukwaani na si uwanjani sehemu ya kuchezea.


Mashabiki kushangilia na wachezaji kwa kuwavamia baada tu ya mechi kunaweza kusababisha madhara mengi sana kwa kuwa wote kwa maana ya mashabiki na wachezaji au watu wa benchi la ufundi wanakuwa na furaha sana au hasira sana.


Mfano, waliovamia uwanja Morogoro hatuwezi kuwa na uhakika, wote ni mashabiki wa Simba. Ni rahisi mchezaji kuumizwa kwa makusudi na wakati mwingine bahati mbaya. Ndio maana hii inakuwa tofauti na ile ya Villa ambao waliingia uwanjani mashabiki wake pia lakini bado naweka msisitizo, haikuwa sahihi.


Mashabiki wa Simba hata wao haiwezi kuwa uhakika hawawezi kuwadhuru wachezaji. Mara ngapi tumewaona wakiwa na jazba na kutaka hata wachezaji wafukuzwe? Kama kuna shabiki alikuwa anamvizia mchezaji siku hiyo amalizie hasira zake?


Kwa kifupi, mashabiki kusogeleana na wachezaji kumekuwa na taratibu zake ambazo zinaufanya kila upande kuwa salama. Ndio maana viwanja vikatengenezwa kwa utaratibu maalum, kwamba huku ni kwa mashabiki ili washangilie vizuri na upande huu ni kwa wachezaji wanapokuwa wanapambana.


Baada ya mechi, mashabiki husogea karibu na mashabiki na kuwapongeza au kuwashukuru kabla ya kurejea vyumbani na si kwenda majukwaani.


Ndio maana unaona wachezaji wanaonywa sana kujumuika na mashabiki, hii ni tahadhari kabla ya hatari. Hata mchezaji akifunga bao, anakatazwa kukimbia upande wa mashabiki kwa kuwa ni hatari.


Baada ya mechi, wachezaji wamechoka, wakati mwingine wanakuwa na hasira, huwezi kujua kama wanaweza kuwa wastaarabu sana mbele ya mashabiki kwa wakati huo. Wanaweza kuwajibu vibaya, wanaweza kufarakana nao na kadhalika.


Bodi ya Ligi na Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), walifanyie kazi hili suala ili kuwapa nafasi makocha na wachezaji nafasi ya kuwa salama zaidi na hili si jambo la kupuuza. Kama mtafanya hivyo ndio kile nimeeleza pale mwanzo kwamba kuchukulia poa, baadaye yakitokea madhara, mtaanza kujilaumu.Pamoja na hivyo, pia mkumbuke, wanahabari wanataka kufanya kazi yao kwa ufasaha na si mazingira yale. Ndio maana wao pia huwa na sehemu zao maalum na wanalazimika kufuata utaratibu ili kuwa hapo. Hivyo mashabiki baada ya mechi wanatakiwa kubaki majukwaani kwa muda au kuondoka kulingana na chaguo lao lakini si kuvamia uwanja tena katika eneo la kuchezea ‘pitch’ ambalo nalo pia wanachangia kuliharibu.


Tulifanyie kazi mapema kabla halijaota mizizi na hatupaswi kuiga madudu kwa kuwa tu yametokea Ulaya.

JIUNGE NA Bin RUWEHY SASA
Usipitwe!! Jiunge nasi kupitia Facebook, Twitter na Instagram ili kupata habari zote za Michezo! Usikose kujiunga na App Yetu Bonyeza HAPA kudownload applicationi ya Bin RUWEHY kwenye simu yako ili kupata habari zetu Haraka